BARUA YA HERMY B KWA MILLARD AYO.
YAH: SABABU ZA MWANA F.A & A.Y KUACHA KUREKODI B HITS
Husika na Kichwa cha Habari;
Ningependa kutoa ufafanuzi wa
habari iliyoandikwa na blog yako kufuatia mahojiano yako na mwana F.A.
Nirejee kwamba mahojiano hayo yanasema kwamba Studio ya kurekodi muziki
ya Kampuni ya Bhits imepandisha bei ya kurekodi, na bei hiyo ndiyo
chanzo cha AY na F.A kuhamishia kazi zao sehemu nyingine.
Baada ya kusoma makala hiyo
inayonihusu mimi binafsi na kampuni ya Bhits kwenye blog yako nimeona
umuhimu wa kujibu makala yako kwani kwa mtu mwingine anaweza kuona ni
kitu cha kawaida lakini kwangu naumia kwa sababu maneno hayo yameshaweka
na yanaendelea kutia hofu wateja wangu hasa hawa wa muziki kwa
kuwafanya wajihisi hawana hicho kiwango cha fedha, kurekodi muziki pale
Bhits.
Naelewa kwamba maneno haya ya
uwongo mtupu yanatokana na mimi kama producer Bhits kushindwana biashara
na AY na FA, lakini sioni sababu ya kuendelea kuongea maneno ya uwongo
na kuniharibia biashara yangu. Sijui nimeawaudhi nini ndugu zangu hawa
mpaka wanataka nionekane mimi nina tabia ya ulafi kwa wasanii wote hapa
Tanzania.
Kitu ambachao hakifahamiki ni
kwamba hata Mwana FA kama ilivyo kwa A.y nae alinitafuta kwa njia ya
simu mwanzoni mwa mwaka huu akinitaka nimuuzie nyimbo zake alizorekodi
kwangu kwa utaratibu wa reja reja kama vile alivyohitaji A.Y, lengo
likiwa ni kuzindua albamu hiyo na kuiuza. Bei aliyotaka kulipa ilikua
pia ni ile ile ya kujilinganisha na msanii mdogo anaehangaika kutoka.
Kitu kingine kilichofanya
tushindwane kibiashara ni pale F.A alipodai bei hiyo ndogo itahusika
katika kumuuzia pia haki zote za muziki huo, yani za kwake na zangu. Kwa
namna nyingine niliombwa nikane haki zangu za muziki kama Producer na
muziki huo uwe mali ya Mwana FA moja kwa moja, akiwa na haki ya kuuza,
kuukodisha na kufanyia biashara yoyote ile anavojiskia yeye bila mimi
kuhusika. Na mimi nikitaka kutumia hata mdundo wa wimbo huo nitahitaji
kumuomba ruhusa yeye labda hata kwa malipo na kinyume cha hapo ana haki
ya kunipeleka mahakamani kunishtaki kwa wizi.
Nilishangazwa kwa kitendo cha
FA kudhani kuwa naweza kukana haki zangu za kimuziki kwa sababu ya tamaa
ya pesa ndogo, nasema kwamba ni hela ndogo ukilinganisha na thamani ya
haki zangu za muziki ambazo huko mbele siwezi jua zitanisaidia vipi.
Mabishano haya ya bei yaliendelea mpaka tukafika sehemu nikamwambia
Mwana F.A anipe Milioni Moja kwa wimbo mmoja ataochukua kwangu kwa ajili
ya albamu yake. Akanambia tuma mkataba lakini aliongeza maneno “bei
yako sio ya kihalisia”. Mkataba huo ulikuwa na kifungu cha kudumisha
urafiki wetu ambacho kinaeleza kuwa, “mauzo ya albamu ni mali ya msanii,
akiamua kunipatia chochote hewala lakini mkataba huu haumlazimu”,
lakini hakusaini mkataba huo.
Nachojiuliza neno kupandishiwa
bei lina maana gani? Kwani si lazima uwe na bei ya mwanzoni ili
inayofata iwe kubwa zaidi? Sasa kama wasanii hawa kwangu walikua
wanarekodi bure na hawalipi hata senti ya umeme wala software ambazo
mimi nimekua nazilipia hela nyingi kwa mwezi kuzifanya zipate leseni ya
kufanya kazi watakua vipi na haki ya kusema wamepandishiwa bei?
Katika barua iliyopita nimesema
kwamba fedha niliyopata kutokana na muziki wao haizidi milioni tatu kwa
miaka yote minne niliyokuwepo nao.
Siifahamu na sijawahi kuwatajia
hiyo bei ambayo inaweza kuwafanya A.Y na F.A warekodi nyimbo za kutosha
hata nje ya Tanzania. Bei ya Bhits wateja wake wanaifahamu na ipo pale
pale kwa kila mtanzania kumudu. Ubora wa muziki wetu wasanii wanaujua
pia na kwa anayependa kurekodi kwetu anakaribishwa kwa kuwa hatubagui na
ambaye hajaridhika na viwango vyetu vya ubora na bei, hili ni soko
huria anaweza kuchagua sehemu nyingine kwa amani kabisa.
Watu wanaweza wakaona mimi ni
mchochezi na mgomvi lakini itambulike hili swala lilikwisha tokea
February mwaka huu nikiwa mimi ndiye niliyeumizwa na nikaamua kukaa
kimya. Nashindwa kuelewa kwa nini wao wameamua kuongelea makubaliano
yetu binfasi kwa media tena kwa kuyageuza maneno.
Itambulike kuwa mara ya kwanza
kabisa hili linasikika kwa media niliwatafuta kwa simu ndugu zangu hawa
nikawaambia kuwa hakuna haja ya Kuongea kwa kuwa yameshakwisha tukae
kimya tulindane. Lakini naona wanaendelea kuongea uongo huo ambao
unaniumiza mimi na kampuni ya B Hits kibiashara.
Biashara zipo nyingi bado na
labda huko mbele tutakutana tena, hakuna haja ya kuharibu kila kitu leo
kwa vitu vidogo kama hivi halafu kesho pia tupoteze nafasi ya kufanya
mambo makubwa, ombi langu ni kwamba tuachane kwa amani. Haswa ukitegemea
hatuna mkataba wa maandishi kati ya mimi, Mwana F.A na A.y nafikiri
kuachana ni kitu rahisi na cha amani na kisichohitaji nguvu wala maumivu
kukitimiza.
Namalizia kwa kusisitiza kuwa niliyoyasema ni ya ukweli na itakaponilazimu kutoa ushahidi nitafanya hivyo.
Wasalaam
Hermes Bariki Joachim (Hermy B)
Managing Director.
No comments:
Post a Comment